1 Corinthians 8

Chakula Kilichotolewa Sadaka Kwa Sanamu

1 aSasa kuhusu chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu, tunajua kwamba “sisi sote tuna ujuzi.” Lakini ujuzi hujivuna, bali upendo hujenga. 2 bMtu yeyote anayedhani kwamba anajua kitu, bado hajui kama impasavyo kujua. 3 cLakini mtu ampendaye Mungu, hujulikana naye Mungu.

4 dHivyo basi, kuhusu kula chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu, tunajua kwamba “sanamu si kitu chochote kabisa duniani na kwamba kuna Mungu mmoja tu.” 5 eKwa kuwa hata kama wapo hao wanaoitwa “miungu” kama wakiwa mbinguni au duniani (kama ilivyo kweli wapo “miungu” wengi na “mabwana” wengi), 6 fkwetu sisi yuko Mungu mmoja, aliye Baba, ambaye vitu vyote vyatoka kwake na kwa ajili yake sisi twaishi na kuna Bwana mmoja tu, Isa Al-Masihi, ambaye kwa yeye vitu vyote vimekuwepo na kwa yeye tunaishi.

7 gLakini si wote wanaojua jambo hili. Baadhi ya watu bado wamezoea sanamu kuwa halisi hivi kwamba wanapokula chakula kama hicho wanadhani kimetolewa sadaka kwa sanamu na kwa kuwa dhamiri zao ni dhaifu, dhamiri yao inanajisika. 8 hLakini chakula hakituleti karibu na Mungu, wala hatupotezi chochote tusipokula, wala hatuongezi chochote kama tukila.

9 iLakini angalieni jinsi mnavyotumia uhuru wenu usije ukawa kikwazo kwao walio dhaifu. 10 jKwa maana kama mtu yeyote mwenye dhamiri dhaifu akiwaona ninyi wenye ujuzi huu mkila katika hekalu la sanamu, je, si atatiwa moyo kula chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu? 11 kKwa njia hiyo, huyo ndugu mwenye dhamiri dhaifu, ambaye Al-Masihi alikufa kwa ajili yake, ataangamia kwa sababu ya ujuzi wenu. 12 lMnapotenda dhambi dhidi ya ndugu zenu kwa njia hii na kujeruhi dhamiri zao zilizo dhaifu, mnamkosea Al-Masihi. 13 mKwa hiyo, kama kile ninachokula kitamfanya ndugu yangu aanguke katika dhambi, sitakula nyama kamwe, nisije nikamfanya ndugu yangu aanguke.
Copyright information for SwhKC